Daily Archives: January 25, 2020

WIZARA YA AFYA ZANZIBAR IMESISITIZWA KUWA NA USIMAMIZI MZURI WA WATENDAJI WAKE HASA KWA WATOTO

Wizara ya Afya imesisitizwa kuwa na usimamizi mzuri wa  Watendaji wake hasa kwa  Watoto wanaozaliwa wakiwa na matatizo ili kupunguza idadi ya vifo kwa watoto.

Wakitoa Majumuisho ya Ziara ya Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Wajumbe wa Kamati hiyo wamesema bado kunatatizo katika Utendaji kwa baadhi ya Wafanyakazi wa Hospitali hasa katika kuwashughulikia Watoto wenye matatizo hayo.

Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya wamesema wanafanya juhudi kurekebisha matatizo katika Hospitali pamoja na vituo vya Afya ili kutoa Huduma bora kwa Wananchi licha ya matatizo kadhaa yakiwemo yanayosababishwa na baadhi ya watendaji wao .

Wakati huo huo Waziri wa Afya Mh.Hamad Rashid Mohamed ametiliana saini na Balozi wa heshima wa Jamhuri ya Cuba Lucas Domingo Hernandez Polledo makubaliano ya kuweka sawa maeneo yaliyokuwa hayamo katika makubaliano ya awali yakiwemo ya utafiti na kuwaongezea utaalamu Madaktari wa Zanzibar.

MKUU WA WILAYA YA KASKAZINI “b” AMEITAKA JAMII KUSHIRIKIANA NA UONGOZI WAKATI WA KUUZA MAENEO

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini " b "Nd. Rajab Ali Rajab ameitaka Jamii kushirikisha Uongozi wa Shehia wakati wa kufanya mauziano ya Maeneo  ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kuepukika ili taarifa zao ziweze kufahamika katika Ngazi ya Serikali za Mitaa.

Wito huo ameutoa   mara baada ya kutembelea  Eneo lenye mgogoro wa mipaka  baina ya Nd.Juma Ussi Juma  na Nd:Ismail  Vuai Foumu  liliopo Katika Shehia ya Mgambo.

Kufuatia mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini " b "Nd. Rajab Ali Rajab amemuagiza  Sheha  wa Shehia ya Mgambo  Nd.Khamisi Juma Khamisi  kukaa pamoja na Kamati yake ya Shehia  ili kusuluhisha mgogoro wa Ardhi  katika Shamba hilo  linalojengwa Madrasa.

Hata hivyo  amewataka Masheha  kutumia busara na hekma pindi wanapofanya usuluhishi  wa migogoro ya Ardhi  kwa kujiepusha kufanya upendeleo  kwani katika jamii kuna baadhi ya Watu wamekuwa  karibu na Masheha kwa lengo la kupata Tahfifu  wanapopatwa na matatizo hali ambayo inasababisha baadhi ya Walalamikaji kukosa haki zao .

Mapema wakitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Wilaya Nd.Ismail Vuai Foumu ambae ndiye mlalamikaji amesema awali Nd.Juma Ussi Juma alimuagiza msimamizi wa Shamba kuwa anataka kununua eneo hilo  na yeye kukataa kumuuzia  kwani Shamba hilo ni Wajukuu wa Marehemu Baba  yake.

 

 

MH MJAWIRI AMEITAKA KAMPUNI INAYOTENGENEZA BOTI YA SEHEWA KUMALIZA KAZI KWA MUDA WALIOKUBALIANA

Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Mh.Mmanga Mjengo Mjawiri ameitaka Kampuni inayotengeneza Boti ya Sehewa kufanya kazi kwa muda waliokubaliana kukamilisha Boti hiyo.

Akizungumza na Ujumbe wa Kampuni inayotengeneza Boti hiyo  Hairunaval  Craft ya Srilanka amesema juhudi hizo zinafanywa kwa Ujumbe huo umemuhakikishia Waziri Mjawiri kuendelea kushirikiana na Serikali mbali na Ujenzi huo wa Boti bali pia katika kuendeleza Sekta ya Uvuvi ikiwemo upatikanaji wa Masoko mazao ya Baharini.

Kampuni ya hiyo ya Hairunaval Craft inaendelea na Ujenzi wa Boti ya Uvuvi na tayari imeshatengeneza Boti ya Sehewa 2 na kukabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

KITUO CHA ZBC KILICHOPO DARE S SALAAM WAMETAKIWA KUWEKA KUMBUKUMBU ZA MAPATO WANAYOINGIZA

Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi  imewataka Watendaji wa Kituo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar kilichopo Dare s salaam kuweka kumbukumbu sahihi  za mapato  wanayoliingizia Shirika  hilo.

Hayo yameelezwa na Wajumbe wa kamati hiyo wakati waalipofanya Ziara ya kukitembelea kituo  hicho ambapo wamewataka Watendaji hao kuwa na Takwimu sahihi, kuziweka wazi na kuepuka kufanya makisio ya fedha wanazozalisha.

Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Mh. Chumu Kombo Khamis  amewataka Wafanyakazi wa Kituo cha  ZBC Dare s salaam kujituma na kuwa tayari kufanya kazi kwa moyo ili kuweza kutoa taarifa zao kwa  ueledi pamoja na kutumia taaluma ya mafunzo wanayopata katika kuandaa kazi zao.

Aidha Wajumbe hao wa Kamati wamewapongeza Watendaji katika Kituo hicho kwa kufanya kazi zao kwa moyo wa kujitolea na kutoa Taarifa za matukio mbali mbali yanayotokea Tanzania

Akitoa Taarifa ya Utendaji kwa kipindi cha miezi sita kwa Kamati hiyo  Kaimu Mkuu wa Kituo cha ZBC  Dare s salaam Nd .Amina Juma amesema jukumu la kituo cha ZBC Dare s salaam ni kuhakikisha kinatafuta, kinakusanya na kuandaa Habari na matukio muhimu yanayotokea kwa upande wa Tanzania Bara ya kiwemo ya Kiuchumi ,Kisiasa ,Utamaduni na Michezo lengo ni kuhakikisha kuwa Wananchi wa  Zanzibar wanapata habari kwa wakati.

Wakati huo huo Kamati pia ilitembelea Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TNS)na kupata nafasi ya kuuliza masuala mbali mbali yanayohusiana na Kampuni  hiyo na  kuishauri kuanzisha Gazeti litakalo kuwa na maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu wa Macho ili kuweza kupata taarifa .

 

error: Content is protected !!