Daily Archives: December 5, 2019

ZANZIBAR INA MENGI YA KUJIFUNZA KUTOKA VIETNAM K

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo Ikulu Mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na  Mjumbe na Katibu wa Kamati Kuu ya Uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV) Bwana Pham Minh Chinh akiwa amefuatana na ujumbe wa viongozi kutoka Chama hicho.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kwamba nchi hiyo imepata mafanikio makubwa katika nyanja zote zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa na kueleza kuwa Zanzibar itaendelea kujifunza kutoka nchi hiyo.

Rais Dk. Shein aliipongeza Vietnam kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo ambao umeweza kuleta mafanikio makubwa sambamba na mahusiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV).

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ziara ya kiongozi huyo hapa nchini inaimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Vietnam na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar pamoja na vyama vikuu vinavyotawala katika nchi mbili hizo.

Alieleza kuwa uhusiano huo ulianza tokea mwaka 1965 kati ya Vietnam na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeweza kuleta manufaa katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo kilimo, uwekezaji, elimu, biashara pamoja na sekta nyenginezo.

Rais Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM, kitaendeleza urafiki na udugu uliopo kati yake na Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV) ikiwa ni pamoja na kuendelea kutembeleana kati ya viongozi wa vyama hivyo na wale viongozi wa Serikali.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein hakuchelea kumueleza kiongozi huyo hatua nzuri na mafanikio yaliopatikana katika ziara yake aliyoifanya nchini humo mnamo mwaka 2012 kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Troung Tan Sang.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika ziara hiyo alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Rais  wa nchi hiyo pamoja na viongozi wengine wakuu na kujadili masuala mbali mbali yaliyojikita kukuza uhusiano na ushirikiano wa pande mbili hizo ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya kilimo, uvuvi, utafiti, biashara na sekta nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi hiyo kutokana na kuendelea kukua kwa uchumi wake pamoja na kuendelea kuwepo kwa amani, utulivu na usalama ambao umeweza kuipaisha nchi hiyo katika nyanja za Kimataifa hatua ambayo inafaa kuigwa na mataifa mengine.

Alimueleza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na inafarajika kuona nchi nyengine zinakuwa na amani kwani panapokuwa na amani maendeleo hupatikana kama ilivyo Vietnam, ambapo aliahidi kuendelea kushirikiana katika sekta za maendeleo ikiwemo biashara, kilimo na uwekezaji.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo Kuipongeza Serikali ya Vietnam na chama chake cha (CPV) kwa kuwahamasisha wawekezaji wa Kampuni ya Halotel kutoka nchini humo kuja kuekeza Tanzania katika sekta ya mawasilianio.

Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa wafanyabiashara wa Zanzibar bado wanaendelea kufanya biashara nchini humo hasa biashara ya mchele hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo ni ya pili duniani katika uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Nae  Mjumbe na Katibu wa Kamati Kuu ya Uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV) Bwana Pham Minh Chinh alimpongeza Rais Dk. Shein kwa mafanikio makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kiongozi huyo wa chama cha (CPV) alimueleza Rais Dk. Shein kuwa nchi yake inaona fahari mkubwa kuwepo kwa mashirikiano na uhusiano mwema kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ni rafiki mkubwa wa Vietnam kwani imeweza kuiunga mkono nchi hiyo katika mambo mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwa ni pamoja na suala zima la usalama kupitia Umoja wa Mataifa (UN) sambamba na kuunga mkono mapambano katika uvamizi wa nchi yao.

Aidha, kiongozi huyo wa chama cha (CPV), alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ziara yake hiyo yeye na viongozi wengine wa chama hicho hapa nchini ina lengo la kukuza uhusiano, ushirikiano na udugu uliopo kati ya (CPV) na (CCM), pamoja na mahusiano kati ya Serikali za nchi hizo.

Pamoja na hayo, kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein jinsi nchi hiyo ilivyopata mafaniko na kupiga hatua katika kuimarisha uchumi wake sambamba na uendelezaji wa amani na utulivu huku kiongozi huyo akisisitiza haja ya kuendeleza utamaduni wa kutembeleana kati ya viongozi wa vyama hivyo na Serikali kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo.

WATOTO WENYE UPUNGUFU MKUBWA WA VITAMINI HUATHIRIKA ZAIDI KWA KUPATA MAGONJWA NA WENGINE HUFA .

Naibu  Waziri  wa  Afya   Mh  Harousi  Said  amesema utafiti  unaonesha  kuwa  watoto  wenye  upungufu mkubwa wa  vitamini   huathirika  zaidi  kwa   kupata  magonjwa   na  wengine  hufa .

Akizungumza  na  waandishi  wa  habari   juuu ya    uzinduzi  wa  matone  na  dawa  za  minyoo  kwa  watoto  walio  chini  ya    umri  wa   miaka  5 amesema   vifo  vya  watoto  huweza  kupungua  kwa  asilimia  23  hadi  30   iwapo  watapatiwa  vitamin  a  kwa  kutumia  vyakula  na  vidonge  vya  nyongeza.

Amesema  ni vyema   wakapatiwa  elimu  ipasavyo  wazazi na   walezi  juu  ya  umuhimu  wa   matone  hayo  ili  kuokoa  maisha  ya  watoto  nchini.

Mkuu  wa  kitengo  cha  lishe  Bi  Asha   Hassan  Salmin  amesema   hali  ya  utapiamlo   hivi  sasa  iko  vizuri  kutokana  na jamii  kuhamasika  katika  hali  ya  unyonyeshaji  ambako  kunahitajika   kushajihishana  ili  kufikia  kiwango  cha  ulaji  kwa   watoto  kunakochangia  kutolewa  kwa   virutubisho  vya  nyongeza  ili  kuwa  na  makuzi  bora  ya  mtoto.

Zoezi  la  utolewaji  wa  matone  na  dawa  za  vitamin  a  hutolewa  mara  mbili  kwa  mwaka  unaohusisha  watoto  waliochini  ya  umri  wa  miaka   5 ambapo  kwa  awali  hii  linatarajia  kuanza  kesho  katika  vituo  vyote  vya  afya  nchini.

 

WALIMU WASTAAFU WAPO TAYARI KUTOA MSAADA KWA WALIMU WANAOENDELEA NA FANI YA UWALIMU

Walimu wastaafu wa skuli ya Sekondari Haile Selassie wamesema wapo tayari kutoa msaada kwa walimu wanaoendelea na fani hiyo Zanzibari ili kukuza kiwango cha elimu nchini.

Walimu hao wamesema ingawa sekta hiyoinabadilika mara mara kwa mara lakini yapo masuala wanayoweza kusaidia hasa katika kujenga wanafunzi wenye tabia njema katika jamii.

Aidha wameomba wananchi kutoa ushirikiano kwa walimu ili waweze kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi pamoja na kuwa waangalizi wazuri wa watoto wao na vitendo vya udhalilishaji

ZANZIBAR HEROES KUSAFIRI KWENDA NCHINI UGANDA KUSHIRIKI MICHUANO YA CHALLENG CUP

Kikosi cha timu ya Taifa Zanzibar (Zanzibar Heroes) kimesafiri nchini Uganda kushiriki michuano ya Challeng Cup yanayotarajiwa kuanza disemba 7 jijini Kampala.

Heroes imeondoka na wachezaji 23 kati ya 35 waliotangazwa na kocha Hemedi Suleiman Moroco huku wachezaji Ibrahim Ame Mohamed [varane] pamoja na Suleiman Said Juma wakisubiri kukamilisha taratibu za vibali vya kusafiri.

Wachezaji hao wakiongozwa na kaimu katibu wa baraza la michezo BTMZ Suleiman Pandu Kweleza.

Awali kikosi hicho kilicheza mchezo wake wa mwisho ikiwa ni sehemu ya kukiaga katika uwanja wa Amani  huku kocha Morroco pamoja na baadhi ya wachezaji wameelezea matumaini yao ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Wakati huo huo tasisi ya mfuko wa jamii Zanzibar ZSSF imekabidhi shiling milioni tano katika shirikisho la soka ZFF kwa ajili ya kusaidia kikosi hicho cha Zanzibar Heroes.

error: Content is protected !!