Monthly Archives: December 2019

WANAFUNZI NA WATENDAJI WA SERIKALI WALIOSOMA NCHINI CHINA WANAJUKUMU KUBWA LA KUITUMIA ELIMU WALIOIPTA KUHAMASISHA MAENDELEO

Waziri wa fedha na mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa amesema wanafunzi na watendaji wa Serikali waliosoma nchini China wanajukumu kubwa la kuitumia elimu walioipta kuhamasisha maendeleo ya uchumi na kijamii visiwani Zanzibar.

Balozi Mohamed Ramia akizungumza katika mafunzokwa wanafunzi waliopata udhamini wa masomo kutoka china amesema nchi hiyo imekuwa ikitoa nafasi za udhamini wa masomo katika kada mbali mbali kwa lengo la kuisaidia Zanzibar kupiga hatua za kimaendeleo .

Amefahamisha China imekuwa rafiki wa muda mrefu kwa Zanzibar hivyo Serikali itaendelea kuthamini ushirikiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili.

Balozi mdogo wa China nchini Tanzania amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita china imetoa nafasi 126 za udhamini wa masomo kwa ngazi ya shahada na nafasi 700 kwa mafunzo ya muda mfupi katika kada  za kilimo, uchumi, mawasiliano, uwekezaji elimu na afya.

Wanafanyakazi na wanafunzi waliopata udhamini wa masomo kotoka China wameahidi kuitumia uzoefu walioupata katika kipindi chote cha masomo nchini china kwa kubuni miradi mbali mbali yenye lengo la kuisadia Zanzibar kufikia uchumi wa kati.

SUMAIT KUWA NA HADHI YA KIMATAIFA KATIKA SEKTA YA UFUNDISHAJI NA UTAFITI.

 

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-sumait Mh: Abeid Amani Karume ameuomba uongozi wa chuo hicho kutafuta njia zaidi ya kukuza chuo hicho kuwa na hadhi ya kimataifa katika sekta ya ufundishaji na utafiti.

akizungumza katika mahafali ya 19 ya chuo hicho huko Chukwani amesema chuo cha Sumait kimekuwa kikitoa taaluma kwa muda mrefu ambayo imeimarika zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma hivyo ni vyema kuangalia njia za kutanua zaidi huduma zao kuwa za kimataifa.

Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya amali Mh: Simai Moh’d Saidi akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo amewaomba wahitimu hao kuwa wazalendo wa Nchi yao pale wanapopata fursa za ajira nje ya Nchi.

Mahafali hayo yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, ambapo jumla ya wahitimu 354 wametunikiwa vyeti vyao ikiwa 237 wahitimu wa stashahada, 59 shahada na cheti 58.

KIJIJI CHA PAJE KUJENGWA UWANJA WA KUTUA HELKOPTA

 

Wizara ya ujenzi, mawasiliano na usafirishaji imesema inafuatilia kupatikana kwa umiliki wa ardhi katika eneo linalotarajiwa kujengwa uwanja wa kutua Helkopta katika kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja.

Waziri wa ujenzi, mawasiliano na usafirishaji, Dkt. Sira Ubwa Mamboya, akizungumza mara baada ya ziara ya kukagua eneo hilo ameutaka uongozi wa mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar kuendelea kufuatilia umiliki huo kwa vile wananchi tayari wameshalipwa ili utarati za ujenzi zianze.

Afisa miradi kutoka mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar, Hafsa Ali Mbaruk, amesema ujenzi huo umekuja kutokana na kukua kwa sekta ya usafiri wa anga pamoja na sekta ya utalii ambapo mamlaka imeona ipo haja ya kujenga kiwanja hicho ambacho kitaweza kutua helkopta ili kurahisisha usafiri.

Amesema uwanja huo utawanufaisha watalii na wananchi wanaotumia usafiri wa anga kwa njia ya Helkopta kutoka uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume hadi uwanja wa Paje

MWANASHERI MKUU WA SERIKALI AMEWATAKA WAFANYAKAZI KUFANYAKAZI KWA UADILIFU, NIDHAMU NA UWAJIBIKAJI

Wafanyakazi wa afisi ya Mwanasheri Mkuu wa Serikali wametakiwa kufanyakazi kwa uadilifu nidhamu na wajibikaji ili lengo la Serikali la kuwapatia huduma bora wananchi liweze kuifikiwa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Nd Said Hassan Said ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi hao katika hafla ya kuwaaga watendaji wawili waliokuwa wa  ofisi hiyo waliyostaafu kazi kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma ya Zanzibar.

Amesema ni heshima kwa mtumishi  kumaliza muda wake wa utumishi kwa nidhamu sambamba na kuwacha  sifa njema za utendaji katika sehemu yake ya kazi ambayo itawajengea heshima watakapokuwa  pamoja na jamii.

Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesifu utendaji mzuri wa wastaafu hao ambao umepelekea kutunza siri za ofisi kutokana na usimamizi mzuri wa kazi zao muda wote walipokuwa kazini.

Kwa upande wao wastaafu hao wamewataka vijana kusimamia majukumu yao kwa uwadilifu na kuepuka udanganyifu na malumbano kazini kwani Serikali na jamii bado inawategemea .

Aidha wamesema ustahamilivu na uwajibikaji ndio kilichowasaidia hadi kufikia kustaafu kwa salama.

Watendaji wa afisi ya Mwanasheria Mkuu waliwatunuku  zawadi wastaafu hao ikiwa ni ishara ya upendo waliouwonyesha muda wote walipokuwa kazini.