Daily Archives: October 15, 2019

VIJANA NA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA MWALIM NYERERE MIAKA 20 ILIOPITA

Vijana nchini wametakiwa kuwa wazalendo, kupenda kazi na kuchukia rushwa kama njia mojawapo ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi (CCM) wilaya ya Mfenesini kichama Charles Lubege wakati wa ziara ya kuwatembelea wazee, watoto yatima na watu wanaoishi katika mazingira magumu katika shehia ya Chuini.

Zoezi hilo liloandaliwa na Baraza la Vijana la shehia hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya sheha wa shehia ya Chuini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya vijana na kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere kilichotokea miaka 20 iliyopita.

Lubege alisema ili kumuenzi na kuziishi falsafa za mwalimu, vijana na wananchi kwa ujumla hawana budi kuendeleza misingi iliyoasisiwa na kiongozi huyo.

Alisema katika maisha yake hayati Baba wa taifa na viongozi wenzake waasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walichukia, kukemea na kutekeza kwa vitendo vita dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi jambo linalopaswa kuendelezwa na kila mwananchi wa Tanzania.

“Mwalimu (Nyerere) na viongozi wenzake walichukia rushwa na aina zote za ubaguzi hivyo ni wajibu wetu sote hasa nyinyi vijana kuyaishi mawazo ya kiongozi huyu ili kumuenzi”, alisema.

Aidha aliwapongeza vijana hao kwa kuamua kuadhimisha siku hiyo kwa kuwatembelea wazee na watu wenye mahitaji akisema kufanya hivyo ni kuendeleza kazi iliyoasisiwa na Rais wa kwanza ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mzee Abeid Amani Karume.

“Hayati Karume (Abeid Amani) na mwenzake Nyerere (Julius Nyerere) waliwapenda na kuwaenzi wazee kwa kuwapatia makaazi na huduma mbali mbali jambo ambalo limeendelezwa na awamu nyengine za uongozi wa Tanzania bara na Zanzibar”, alisema Lubege.

Awali akisoma risala ya Baraza la vijana wa shehia ya Chuini Mbaraka Suleiman alisema ziara hiyo imelenga kuwaenzi wazee hao na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

“Tumeamua kuadhimisha siku hii kwa kuwafikia wazee na vijana wetu ili kutambua mchango wao katika ujenzi wa taifa na kuwapunguzia majonzi kama ilivyokuwa wakati wa mwalimu Nyerere ili kutuongezea ari na morali ya uzalendo na mapenzi kwa nchi yetu”, alisema mbaraka.

Nae Sheha wa shehia hiyo Mohammed Shehe Kheir alieleza kuwa ziara hizo zitakuwa endelevu na kuwaomba wadau mbali mbali kuendeleza mema yaliyoasisiwa na viongozi hao.

“Tumeamua kuiadhimisha siku hii kwa namna hii ili kuongeza uimara wa vijana wetu katika kupenda nchi yao na watu wake, kwa kuzingatia umoja na mshikamano wa nchi yetu”, alisema sheha Kheir.

Nao wanufaika waliofikiwa katika ziara hiyo waliwashukuru vijana hao kwa kuwatembelea na kuwahilmiza kuendelea kuwa waaminifu na waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tunawashukuru kwani vitu mlivyotupatia vitatusaidia kwa siku chache lakini mnatukumbusha namna viongozi wetu walivyowalea kwa ajili ya nchi na watu wake”, alisema mzee Omar Juma Kombo (65).

Katika ziara hiyo kaya zaidi ya 30 zilifikiwa na kupatiwa vitu mbali mbali vikiwemo vyakula, nguo na sare za skuli vyenye thamani ya shilingi Milioni 2.8 ikiwa ni mchango wa wanachama wa baraza la vijana na uongozi wa shehia ya Chuini wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja

error: Content is protected !!