Daily Archives: February 8, 2019

MATAIFA YOTE ULIMWENGUNI YANAPASWA KUWA NA MFUMO MMOJA WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

Rais wa taasisi inayosimamia mazingira ya umoja wa mataifa bwana Siim Valmar Kiislar amesema mataifa yote ulimwenguni yanapaswa kuwa na mfumo mmoja wa utunzaji wa mazingira utakaosaidia kuifanya dunia iendelee kubakia salama.

Amesema tabia ya baadhi ya mataifa kuendelea kukwepa mikataba na baadhi ya kanuni zinazowekwa kimataifa pamoja na kuweka vikwazo vyenye nia ya kulinda maslahi yao binafsi vitapelekea kuongezeka kwa wasiwasi utakaoifanya dunia hii ibakie katika mazingira hatarishi.

Bwana Siim Valmar Kiislar alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika ofisi yake iliyomo ndani ya jengo laBaraza la wawakilishi liliopo Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Rais huyo akiuongoza ujumbe mzito wa taasisi hiyo ya mazingira ya umoja wa Mataifa amekuja kushuhudia uzinduzi wa kampeni ya kidunia ya uzinduzi wa usafi wa mazingira katika fukwe ya Forodhani Visiwani Zanzibar ulioambatana na ujio la mashua ya mazingira iliyotengenezwa kutokana na malighafi ya plastiki kutoka nchini Kenya.

Bwana Siim Valmar ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa umakini wao wa kusimamia masuala ya mazingira katika kuitikia kampeni ya kimataifa ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema kitendo cha zanzibar kufanikiwa katika mapambano yake ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki mbali ya kuwa mfano kwa mataifa ya ukanda wa afrika mashariki na kusini mwa afrika, lakini pia kimeleta faraja kwa umoja wa mataifa kupitia taasisi yake hiyo  inayosimamia masuala ya mazingira.

Naye mratibu mkaazi wa mashirika ya umoja wa mataifa yanayofanya kazi nchini tanzania bwana Alvaro Rodriguez alisema bado mataifa ulimwenguni yana wajibu wa kushirikiana katika mapambano yake dhidi ya uchafuzi wa mazingira.

Bwana Alvaro alisema ustawi wa jamii pamoja na viumbe vilivyomo  ndani ya dunia vitaendelea kuishi kwa amani bila ya vikwao endapo ushirikiano huo utaimarishwa na kuendelea kuwa wa kudumu kama inavyoonekana katika baadhi ya maeneo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar bado inaendelea kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi akatolea mfano ufukwe wa bahari ya msuka uliopo kaskazini mwa kisiwa cha pemba ambao tayari umeshaliwa na mawimbi ya bahari kwa sehemu kubwa.

Balozi Seif aliueleza ujumbe huo wa taasisi ya umoja wa Mataifa unaosimamia mazingira kwamba zanzibar imeanza mikakati ya kupiga marufuku matumizi na uingizwaji wa mifuko ya plastiki tokea mwanzoni mwa miaka ya 90 na kufanikiwa vyema katika azma yake ya kulinda mazingira.

Alisema ujio wa mashua ya mazingira katika visiwa vya Unguja na Pemba utasaidia mfano wa darasa kwa wananchi waliowengi kuwa na muelekeo wa jitihada za mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumbwa dunia hivi sasa na kuleta athari kubwa ya kimazingira.