Daily Archives: January 30, 2019

ZECO YATOA ELIMU KWA WANANCHI WA MSUKA

Wananchi wa shehia ya  Msuka  mashariki wametakiwa kuacha tabia ya kuchimba mchanga, kupanda miti ya kudumu  pamoja na kufanya  harakati  zozote za kijamii katika line kuu za umeme  ili kuepusha athari inayoweza kujitokeza.

Akizungumzana wananchi wa kijiji hicho huko ukumbi wa Skuli ya Haroun Msuka   wakati akitoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya umeme uliozinduliwa hivi karibuni afisa uhusiano wa shirika la zeco Amour Ali Amour amesema si jamabo la busara mtu au watu kufanya kitendo chochote kitachopelekea   uharibifu katika   miundo mbinu ya  huduma ya umeme kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria.

Nae mhandisi wa Shirika la  Umeme Zeco Ali Faki Ali amewataka wananchi kuthamini juhudi zinazochukuliwa na serikali kupitia  shirika la umeme katika kuhakikisha huduma muhimu  za kimaendeleo zinawafikia .

Kwa upande wao wananchi hao wameahidi kushirikina katika kuitunza miondo mbinu hiyo ili iweze kudumu na  kutoa huduma stahiki kwa faida yao na vizazi vya baadae.

 

RAIS MAGUFULI AMEWAPISHA MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI NA MAJAJI WA MAHAKAMA KUU

Rais wa jamuhuri ya muungano wa tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo amewapisha majaji sita wa mahakama ya rufani na majaji 15 wa mahakama kuu aliowachagua mwishoni mwa wiki iliyopita.

Halfa hiyo ya uapisho imefanyika ikulu jijini Dare s salaam na kuhudhuriwa na makamo wa rais mama Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania  Pro. Ibrahimu Khamis Juma, katibu mkuu kiongozi Balozi Kijazi,majaji wastaafu, mawaziri, manaibu waziri ,viongozi wa dini na vyama vya siasa ambapo walioapishwa ni kwa upande wa majaji wa mahakama ya rufani ni Barke Mbaraka Sahel,Dk. Winfreda Korosso,Lugano Mwandambo, Dk. Mary Levira, Ignas Kitusi na Dk. Rehema Sameji

Wengine walioapishwa kuwa majaji wa mahakama kuu ni Cyprian Mkeha,Dustan Ndunguru,Seif Kulita ,Dk. Mtemi Kilikamajenga ,Zefereni Galeba,Dk. Juliana Masabo,Mustafa Ismail,Upendo Maheda,Wilbard Mashauri ,Yohanne Masara,Dk Lilian Mongella, Fahamu Mtulya ,John Kahyoza,Athuman Kirati na Suzan Mkapa.

Akizungumza katika hafla hiyo  Rais  Magufuli amesema majaji  hao wanajukumu kubwa la kusimamia haki na kufanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa na kuwataka kufuata sheria na katiba ya nchi katika utoaji wa maamuzi yao.

Pia Mh. Magufuli amewataka wakuu wa wilaya kutotumia vibaya sheria na mamlaka walizopewa na kufanya kazi kwa kufuata sheria  katiba na kuagiza wakurugenzi kusimamia mapatao na kuacha  mabishano na wakuu wa mikoa na wilaya

Nae  makamo wa Rais Mhe Samia  Suluhu Hassan amewaambia majaji walioapishwa kuwa ana imani wataenda kufanya kazi vizuri na kwa upande wa wakuu wa wilaya waliyochaguliwa  wa tarime na mwanga kwenda kutatua changamoto zilizokuwepo na  kutorudia makosa yaliyotendeka

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Pro. Ibrahimu Khamis Juma amesema idadi hiyo ya majaji wapya imeongeza idadi ya majaji kutoka 66 hadi kufikia 80 idadi hiyo itasaidia kupunguza mzigo wa usikilizaji wa mashauri zaidi 500 hadi 462 kwa jaji mmoja.

Mara baada ya kuapishwa majaji hao pamoja na wakuu wa wilaya wawili aliowachagua  na wakurugenzi 10 waliojaza nafasi zilizokuwa wazi  walikula kiapo cha uadilifu zoezi lililoongozwa na jaji mstaafu aron sekela.

 

 

 

 

 

TAMASHA LA PASAKA KWA MWAKA 2019 LINATARAJIWA KUFANYIKA JIJINI DAR-ES-SALAAM

 

Tamasha la pasaka kwa mwaka 2019 linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 21 april 2019 na kwa mwaka huu litaanzia jijini dares salaam, baadae na maeneo mengine ya nchi

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-salaam, Mkurugenzi wa Msama promotion Alex Msama amesema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri, na kinachoendelea sasa ni mawasiliano na wasanii wataoshiriki wakiwamo wa kutoka nje ya nchi.

Aidha ndugu Msama ameelezea faida za tamasha hilo la pasaka kuwa mbali na kutoa burudani ni kuombea amani na umoja wa watanzania.

Katika kufuata maelekezo ya baraza la sanaa la taifa (basata) ndugu Msama ameelezea mwongozo uliotolewa juu ya wasanii wataoshiriki kwenye tamasha hilo huu kuwa ni wale wenye usajili wa basata hivyo amewasihi wasanii kufuata miongozo ya inayotolewa na chombo hicho.

SMZ KUANZISHA TAASISI YA UTAFITI YA UVUVI NA MAZAO YA BAHARI

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein  amesisitiza azma ya serikali ya mapinduzi ya zanzibar ya kuanzisha taasisi ya utafiti ya uvuvi na mazao ya bahari ili kwenda sambamba na sera ya uchumi wa bahari.

dkt shein ameyasema hayo katika kikao na uongozi wa wizara ya kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi ikulu mjini zanzibar ambapo makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali idd nae amehudhuria.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na Mazao ya Bahari hasa ikizingatiwa mazingira ya Zanzibar na uchumi wake.

Alieleza kuwa ni jambo la busara kuwepo kwa Taasisi hiyo hapa Zanzibar ambayo itakuwa na umuhimu mkubwa kwa Zanzibar pamoja na wananchi wake na kuipelekea Zanzibar kutekeleza ipasavyo uchumi wa bahari kwa vitendo.

Alieleza kuwa tayari Zanzibar ni mwanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA), hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mikakati madhubuti katika kufikia malengo, makubaliano na maazimio ya Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo uchumi wa bahari

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya uwepo wa Jumuiya hiyo ya (IORA) pia, Novemba mwaka jana 2018 alihudhuria Mkutano wa Uchumi wa Bahari uliofanyika mjini Nairobi Kenya kuanzia Novemba 26 hadi 28 ambapo mbali ya mambo mengineyo mkutano huo pia, ulijikita na masuala ya uchumi wa bahari hasa kwa nchi zilizopakana na Bahari ya Hindi.

Rais Dk. Shein pia, alieleza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha viwanda vya uvuvi hapa nchini, azma ya kuanzisha Chuo cha Ubaharia pamoja na kuiimarisha Kampuni yake ya  Uvuvi.

Akieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji maji, Rais Dk. Shein alisema kuwa umefika wakati kwa Zanzibar kuongeza ukubwa wa eneo la kilimo cha umwagiliaji maji kwani mradi huo una umuhimu mkubwa kwa Wazanzibari hasa ikizingatiwa kuwa chakula cha wali ndio kilichopewa kipaumbele na jamii.

Alieleza kuwa matarajio ya Serikali ni kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji wa mpunga kutokana na mradi huo mkubwa.

Aidha, Rais Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Wizara hiyo na kusisitiza kuwa mashirikiano katika kazi ni suala la lazima sambamba na kufanya kazi kwa kufuata maadili, sheria na kanuni za kazi ambayo yanaleta usalama mkubwa kazini.

Akisisitiza suala zima la mashirikiano kazini, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuendelea kuwaongoza vyema watendaji waliochini yao huku akiwaeleza malengo na madhumuni ya kuwepo kwa vyeo na utofauti uliopo kati ya kiongozi na anaeongozwa.

Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja hasa ikizingatiwa kuwa kila mmoja ana majukumu yake hasa wakizingatia kuwa wanaowafanyia kazi ni wananchi.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kufanya kazi kwa juhudi hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na kubeba mambo muhimu katika maisha yao.

Mapema Waziri wa ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Rashid Ali Juma alieleza maendeleo ya mradi wa Usimamizi wa shughuli za Uvuvi wa Kanda ya Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) ambao ni mradi wa miaka sita ulioanza Juni 22,2015 hadi Septemba 2021.

Alieleza kuwa mradi huo umetayarishwa kwa dhamira ya kuongeza faida kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa nchi za Kusini Magharibi mwa Barahari ya Hindi (SWIO) kutokana na matumizi endelevu ya uvuvi wa bahari ambao hivi sasa unatekelezwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania, Msumbiji na Comoro.

Pia, Waziri Juma alieleza kuwa Ujenzi wa Miundombinu ya Umwagiliaji maji unaotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkopo wa Benki ya Exim-Korea ambao ni miongoni mwa juhudi na mikakati ya Serikali kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo.

Pia, alieleza kuwa mradi huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Umwagiliaji maji wa Zanzibar ambapo mkataba wake ulitiwa saini tarehe 6 Disemba 2018 baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya hiyo na Kampuni ya Ujenzi ya KOLON- HANSON JV kutoka Korea utakaogharimu Dola za Kimarekani milioni 64.3.

Aliongeza kuwa Mradi huo utajumuisha ujenzi wa miundombinu ya mitaro ya umwagiliaji, mabwawa manne makubwa, kuchimba visima 49 na kuweka pampu zake, ujenzi wa maeneo ya kuanikia mpunga na kukata vishamba pamoja na kuweka sawa ardhi.

Alieleza kuwa mradi huo utajenga na kuendeleza eneo litakalokuwa na jumla ya hekta 1,524 (Eka 3,810) zitakazojengwa katika mabonde saba ya umwagiliaji maji kwa Unguja na PEMBA ambayo ni Cheju, Kinyasini, Kibokwa, Kilombero,Chaani, Makwararani na Mlemele.

Alisisitiza kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuimarisha usimamizi makini wa uvuvi wa kipaumbele kuanzia ngazi ya Kikanda, Kitaifa na Kijamii.

Pamoja na hayo, Waziri huyo alieleza lengo kuu la usimamizi wa Serikali katika uchimbaji wa mchanga na usafirishaji wake ambalo ni kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo inapatikana kikawaida kwa matumizi ya wananchi na kwa bei nafuu kwa mujibu wa kanuni na Sheria zilizopo.

Uongozi wa Wizara hiyo ulieleza kufarajika na ushauri, maelekezo wanayoyapata kutoa kwa Rais Dk. Shein ambayo yamekuwa chachu katika utendaji wa kazi zao huku wakitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa wataendelea na ushirikiano mkubwa walio nao ili kuweza kuendelea kupata mafanikio makubwa zaidi katika Wizara hiyo.