Daily Archives: January 29, 2019

DK. ALI MOHAMED SHEIN AMEKUTANA NA MABALOZI WA NCHI ZA KUWAIT, ETHIOPIA NA MISRI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amekutana na  kufanya mazungumzo na Mabalozi wa nchi za Kuwait, Ethiopia na Misri ambapo mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano sambamba na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi za kujiletea maendeleo.

Mazungumzo hayo yalifanyika kwa nyakati tofauti Ikulu mjini Zanzibar ambapo Mabalozi hao walifika kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais Dk. Shein,  miongoni mwao ni Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mubarak Mohammed, Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Yonas Yosef na Balozi wa Misri nchini Tanzania Gaber Mohamed.

Katika mazungumzo yao Mabalozi hao walipongeza mafanikio yaliofikiwa Zanzibar na kuahidi kuendelea kuyaunga mkono huku wakitumia fursa hiyo kutoa pongezi maalum kwa Rais Dk. Shein pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa kufanikisha Sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 ambazo zilifana kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza na Balozi wa Kuwait, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo na kuupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi  wa Kuwait kwa kuiunga mkono Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema  nchi ya Kuwait imekuwa ikiiunga mkono na kutoa ushirikiano mkubwa kwa Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu, kilimo na nyenginezo huku akiwakaribisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar .

Nae, Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mubarak Mohammed alieleza azma ya nchi yake ya kuendelea kushirikiana na Zanzibar kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo na kuelezea azma ya kusaidia  kuimarisha sekta za afya, elimu na Kilimo hapa nchini.

Rais Dk. Shein pia, alifanya mazungumzo na  Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Yonas Yosef ambapo katika mazungumzo hayo, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein mafanikio yaliofikiwa na nchi yake kiuchumi, kisiasa na kijamii ikiwa ni pamoja na kukua kwa Shirika  la ndege la ‘Ethiopia Airlines’, pamoja na kurejesha uhusiano kati ya Ethiopia na nchi jirani ya Eritrea.

Aidha, Balozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa kurejea kwa uhusiano kati ya nchi yake na Eletria kutaimarisha shughuli za kimaendeleo sambamba na kukuza hali ya amani katika ukanda wa nchi hizo pamoja na nchi jirani za Sudan, Djibout.

Balozi huyo pia, alimueleza Rais Djk. Shein kuwa kuimarika kwa sekta ya usafiri kupitia Kampauni ya ndege ya ‘Ethiopia Airlines’ , kutaongeza idadi ya watalii wanaofika Zanzibar pamoja na kutoa huduma bora za usafiri kwa wananchi wa pande mbili hizo ambapo pia, Balozi huyo alieleza mafanikio yaliofikiwa na Serikali ya Ethiopia katika kuweka usawa wa jinsia katika nafasi za uongozi.

Nae, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo kuwa  Ethiopia na Tanzania zina historia ya muda mrefu katika ushirikiano na uhusiano tokea wakati wa mapambano ya kudai uhuru ambapo waaasi wa nchi mbili hizo akiwemo Haile Salassie na Mwalimu Julius  Kambarake Nyerere walishirikiana.

Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inathamini sana juhudi za kiongozi huyo ambaye ni muasisi wa Ethiopia katika harakati zake za ukombozi wa Mwafrika na ndio maana Zanzibar ikaweka alama kwa kuiita jina la kiongozi huyo skuli ya Sekondari ya Haile Salassie iliyopo mjini Zanzibar.

Katika maelezo hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa kabla ya ukoloni Bara la Afrika lilikuwa moja na ndio maana hadi hivi leo licha ya kuwepo nchi mbali mbali ndani ya Bara hilo lakini bado Waafrika wote ni ndugu na wamekuwa wakiendeleza ushirikiano wao.

Alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia Abiye Ahmed kwa kurejesha hali ya uhusiano na ushirikiano kati ya Ethiopia na Eritrea hatua itaakyoimarisha maendeleo kati ya pande hizo sambamba na kukuza uchumi na kujenga udugu wa wananchi wake pamoja na wananchi wote wa Bara la Afrika.

Rais Dk. Shein alieleza mafanikio makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar kwa kuwepo huduma za usafiri wa ndege za Kampuni ya ‘Ethiopia Airlines’ ambazo zimeweza kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kuitembelea Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba sekta hiyo ina umhimu mkubwa kwa uchumi wa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa nchi hiyo kufungua Ubalozi wake mdogo hapa Zanzibar huku akipongeza ahadi za Balozi huyo kwa nchi yake kuendelea kutekeleza Makubaliano ya Mkataba kati yake na Tanzania ambayo alisema yatazidi kufungua milango ya ushirikiano.

Wakati huo huo,Rais Dk. Shein alikutana na Balozi wa Misri nchini Tanzania Gaber Mohamed ambaye Balozi huyo alitumia fursa hiyo kumuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Misri itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo, mafunzo na uwezeshaji wa programu mbali mbali kupitia sekta hiyo na nyenginezo.

Balozi huyo wa Misri alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake iko tayari kuanzisha maeneo mengine ya ushirikiano kwa azma ya kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo huku akiahidi juhudi zitaongezeka kushajihisha watalii kutoa Misri kuja kuitembelea Zanzibar.

Aidha, Balozi huyo alieleza hatua zitakazofuata katika kuhakikisha kunakuwepo ushirikiano kati ya wafanyabiashara na wenye Kampuni wa Misri na Zanzibar kwa kuwaweka pamoja kwa lengo la kubadilishana mawazo na kutafuta njia bora za kukuza biashara na uwekezaji.

Nae, Rais Dk. Shein kwa upande wake alitumia fursa hiyo kuipongeza Misri kwa kuendelea kushirikiana na Zanzibar na kueleza kuwa ushirikiano na uhusiano huo ni wa muda mrefu tokea uwepo wa waasisi wa nchi mbili hizo akiwemo kiongozi wa Misri Gamal Abdulnasir ambaye alikuja kuitembelea Tanzania, pamoja na kufika Zanzibar.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Misri kwa kuleta wataalamu hapa Zanzibar wakiwemo wataalamu wa kilimo ambao walisaidia sana kutoa mafunzo ya kilimo hapa nchini huku akisisitiza haja kwa nchi hiyo kuleta wataalamu wakiwemo Madaktari bingwa wa afya kupitia programu maalum.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa Misri kuleta wataalamu katika sekta ya michezo hasa ikifahamika kwamba hapo siku za nyuma nchi hiyo imeshawahi kuleta wataalamu wake na kuja kutoa mafunzo ya michezo hapa nchini hasa kwa timu ya vijana katika mchezo wa mipira wa miguu

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Wanazuoni, Masheghe na Maulamaa wengi wa Zanzibar walipata elimu zao za dini ya Kiislamu kutoka Misri, hivyo ipo haja kuendeleza utamaduni huo wa kushirikiana kati ya nchi hiyo na Zanzibar ili mafunzo hayo ya elimu ya dini yaendelee na kuzidi kuleta tija kwa jamii.

Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Elexandria cha nchini Misri pamoja na kuendeleza mradi wake wa umeme wa kutumia nguvu za jua ambao unaweza kuwa mkombozi wa nishati ya umeme kwa Tanzania pamoja na Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwaahidi Mabalozi hao wote kuwa yeye pamoja na Serikali anayoiongoza wataendelea kufanya kazi nao vizuri kwa lengo na azma ile ile ya kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo na Tanzania ikiwemo Zanzibar.

TABIA YA UTORO KWA WANAFUNZI WA SKULI YA KILINDI YAONGEZEKA

Kuwepo kwa hoteli za kitalii kumeelezewa kuwa bado ni tatizo   linalochangia tabia ya utoro kwa  wanafunzi wa  skuli ya kilindi mkoa wa kaskazini unguja.

Kaimu Mwalimu Mkuu kwa upande wa Skuli ya Msingi wa Skuli hiyo Mohd Haji Makame ameiambia ZBC kuwa tabia hiyo ipo kwa wanafunzi na zaidi  inasababishwa na  tamaa  ya kupata fedha  katika  hoteli za ukanda huo wa pwani.

Amefahamisha kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakiingia katika maeneo  hayo huku wakiwa na biashara tofauti na kuwauzia wageni  na hivyo hupelekea kusahau muda wao wa masomo .

wamesema  tabia  ya utoro katika skuli hiyo  inashamiri zaidi  msimu wa wageni  wanapokuwa wengi ambao ni  mwezi wa march, april  na may na kusema kuwa  hata hivyo skuli  itaendelea kupokea  wanafunzi wenye tabia hiyo ili kuendelea na masomo.

Abdalla  Ali Ali ni  mtakwimu mkuu wa Skuli ya Kilindi  amesema  idadi hiyo ya utoro katika skuli hiyo  imekuwa kubwa kwa wanafunzi wa  msingi ambapo  sekondari hali   ya utoro inaridhisha.

Mwalimu wa Skuli hiyo Rukia Iddi Mohd   amesema  kuwepo kwa tatizo hilo kunasababshwa  na  mwamko mdogo wa Wazazi juu ya Watoto wao  na kuishauri wizara  na kamati za elimu kusimamia vyema  matatizo  yanayoikumba skuli hiyo.

              

SEKTA YA UVUVI KUSHIRIKISHWA PALE WANAPOFANYA MAREKEBISHO AU UANDAAJI WA SHERIA

Fungamano la vyama vya sekta ya uvuvi wa ukanda wa pwani  tanzania umeiomba serikali kuwashirikisha wadau wa sekta ya uvuvi pale wanapofanya marekebisho au uandaaji  wa sheria na kanuni ili kuondoa changamoto  iliyopo katika sekta hiyo.

Ushauri huo umetolewa na wadau wa sekta ya uvuvi walipokuwa wakiwasilisha kero wanazokabiliana nazo katika shughuli zao za kila siku kwa watendaji wa afisi ya uratibu wa shughuli ya serikali ya mapinduzi ya  Zanzibar iliyopo Dar es salaam ambapo wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo  utozwaji wa faini usiofata taratibu,kukamatwa kiholela na kunyanyaswa kwa vipigo,kuchomewa moto dhana zao za uvuvi .

Wakizungumza kero hizo baadhi ya wavuvi na wamiliki wa vyombo walikuwa na haya ya kusema.

Nae afisa uratibu  kutoka afisi ya uratibu wa shughuli ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anaeshughulikia masuala ya kilimo ,uvuvi na maliasili Bi Mwanaisha  Ramadhani Kondo  amewahakikishia wadau hao kuwa kero walizozieleza zitafikishwa katika mamlaka husika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Akisoma taarifa hiyo mratibu wa fungamano wa vyama vya sekta ya uvuvi Nd. Mahammed Said Muhidini ameomba mamalaka husika kuwakutanisha na rais wa jamuhuri ya muungano wa tanzania Mh. John Pombe Magufuli kuzungumza nao kuweza kupatiwa ufumbuzi kero zao kama zilizofanya katika taasisi nyengine zikiewemo za madini na wakulima wa korosho.

Kikao hicho kiliwashirikisha wadau mbli mbali wa sekta ya uvuvi wakiwemo wamiliki wa vyombo,wavuvi na  manahodha pamoja na maafisa kutoka ofisi ya uratibu wa shughuli za SMZ wanaosimamia kilimo, mifugo uvuvi na mali asili pamoja biashara na uwekezaji.