Daily Archives: January 28, 2019

MSIKITI NI NYUMBA YA MWENYEZI MUUNGU INAYOWAKUTANISHA KUTEKELEZA NGUZO YA PILI YA DINI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Waumini wa Dini ya Kiisalamu kuelewa kwamba msikiti ni nyumba ya mwenyezi muungu inayowakutanisha kutekeleza nguzo ya pili ya dini hiyo inayojumuisha pamoja na mambo mengine Ibada ya sala, Elimu, Maarifa  pamoja na Malezi kwa Watoto.

Amesema katika kutekeleza hayo Waumini hao wanapaswa kuwa madhubuti katika kuilinda Misikiti  kutokana na madarasa ya uchochezi yaliyoibuka katika baadhi ya sshemu Nchini ambayo huwa na muelekeo wa kuwagawa Waumini Kibadhehebu au Kisiasa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Msikiti Salama { Masjid Salama } uliojengwa kwa nguvu za Waumini wenyewe wa Dini ya Kiislamu pamoja na misaada ya Wahinsani katika Mtaa wa Maungani Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa Mjini Magharibi.

Alisema Jamii imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la dhulma na mmong’onyoko wa Maadili unaochangiwa na vitendo vya Ubakaji, Ulawiti, udhalilishaji wa Watoto Wadogo, Utumiaji wa Dawa za Kulevya kwa kiwango cha kutisha mambo yanayosababishwa na upungufu wa Maadili yanayopaswa kutiliwa mkazo hasa kwenye madarasa Misikitini.

Balozi Seif aliwaomba Waumini na Wananchi wote Nchini kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika kuondosha maasi hayo yaliyokithiri na kutishia Imani za waja ambayo tayari yameshakemewa na Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad {SAW}.

Alieleza kwamba Msikiti ni Nyumba isiyo na mbadala kutokana na utukufu wake. Hivyo aliwanasihi  Wana Maungani kutumia Mali na nguvu zao zote katika kuutunza ili ubakie Mpya, wakupendeza ili uendelee kuhudumia kazi ya mola ya kuabudiwa na Viumbe vyake.

Akisoma Risala Mjumbe wa Kamati ya Masjid Salama Dr. Ali Uki alisema baadhi ya  Waumini wa Kijiji cha Maungani walilazimika kufanya Ibada zao ndani ya Majumba yao hasa kwa ile Sala ya Alfajiri kutokana na umbani wa Msikiti uliopo kwenye eneo hilo kwa kuhofia kiza kilichotanda katika eneo hilo.

Dr. Uki alisema usumbufu huo uliwapa fikra iliyozaa maarifa ya kuanza ujenzi wa Jengo lao la Ibada ili kuondokana na kadhia hiyo iliyopelekea jitihada zao kuzaa matunda ya kuanza ujenzi ndani ya kipindi cha Miaka Mitano iliyoanzia Mwezi Mei Mwaka 2014.

SMZ HAITOSITA KUMUWAJIBISHA MTENDAJI ATAKAYEHUSIKA NA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba serikali haitosita kumuwajibisha mtendaji yeyote wa halmashauri   atakayehusika na matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa jimbo zinazotengwa kwa ajili ya kuendeleza miradi ya wananchi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati alipozindua rasmi mradi wa maji safi na salama katika skuli ya msingi mangapwani ambao pia utasaidia kusambaza huduma hiyo katika vijiji jirani vinavyoizunguuka skuli hiyo.

Amesema wapo baadhi ya watendaji ndani ya halmashauri za wilaya wakionyesha udhaifu wa kuzorotesha miradi ya wananchi waliyoianzisha ilhali fedha zinazotengwa kuitekeleza miradi hiyo huwa tayari zimeshaidhinishwa na kutiwa saini na viongozi wanaouhusika.

Balozi Seif amesema kuanzia sasa atalazimika kufuatilia changamoto zote anazowasilishiwa zinazohusiana na kadhia hiyo na hatosita kumchukulia hatua za kinidhamu mtendaji atakayebainika kuhusika na hadaa yoyote hasa ile inayohusiana na masuala ya fedha.

Aliwataka wananchi wa mangapwani kutoa taarifa mapema pale yanapojitokeza matatizo ya kiufundi katika uendeshaji wa mradi huo wa maji safi na salama na kuacha tabia ya kuwatumia mafundi wa vichochoroni wanaoweza kuleta athari zaidi ya kiufundi kwenye mradi huo muhimu kwa ustawi wa jamii.

USAFI NI SEHEMU YA KUEPUSHA KUTOKEZEA BAADHI YA MARADHI

Kazi za usafi zinazofanywa na baadhi ya taasisi za kujitolea katika hospitali kuu ya mnazi mmoja zimekuwa ni sehemu ya kuepusha kutokezea baadhi ya maradhi yanayosababishwa na hali ya uchafuzi wa mazingira.

Miongoni mwa waliojitolea kufanya kazi ya usafi wa mazingira katika hospitali hiyo ni, ni jumuiya ya umoja wa mataifa ya vijana ya chuo cha kumbu kumbu ya mwalimu nyerere.

Akizungumza mkurugenzi utawala na uendeshaji katika hospitali kuu ya mnazi mmoja Nd. Abubakar Khamis Hamad, amesema uongozi umepata faraja kuona baadhi ya taasisi zinajali maisha wagojwa na wanaopatiwa huduma katika hospitali hiyo.

Mbali na kufanya usafi jumuiya hiyo pia imetembelea wodi ya watoto waliolazwa katika jengo la dodoma wakiongozwa na rais wa serikali ya wanafunzi badru suleiman badru na mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa mataifa ya vijana mohamed ali ramadhani.